Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Homa ya Kichaa cha Mbwa


Utangulizi

Kichaa cha mbwa ni nini?

Ni ugonjwa hatari unaotokana na maambukizi ya virusi vijulikanavyo kama rabies kwa kiingereza. Maambukizi hayo hutokea baada ya kung'atwa, kukwaruzwa na makucha au kulambwa machoni,puani, mdomoni au katika jeraha na mbwa, paka  au popo aliye na virusi hivyo. 

Tofauti na virusi,unapong'atwa na mbwa au paka ni hatari ya kupata maambukizi ya bakteria katika majeraha ambayo husababisha maumivu makali na kuchelewesha kupona kwa majeraha hayo kama hatua hazitachukuliwa haraka. Lakini pia kupata majeraha sehemu za viungo(joints) kunaweza kumsababishia mgonjwa ulemavu wa kudumu.

Nchini Tanzania pekee inasadikiwa kuwa watu 1500 hufariki kila mwaka kutokana na kichaa cha mbwa, ugonjwa unaoweza kuzuiwa kwa asilimia 100 kwa kutumia chanjo(DW).

Nini cha kufanya unaposhambuliwa na mbwa, paka au popo?

 Kuna hatua muhimu kadhaa za kufanya pindi unaposhambuliwa na mbwa, paka au popo.
  1. Safisha majeraha kwa maji yanayotiririka na sabuni bila kusugua kwa dakika tano hadi kumi,
  2. Paka  mafuta ya antibayotik kama unayo, epuka kupaka mafuta ya mgando,mafuta ya taa, mkojo au kitu kingine chochote zaidi ya mafuta ya antibayotik,
  3. Punguza kutokwa na damu kwa majeraha kwa kufunga kwa kipande kisafi cha nguo au bandeji mpaka pale utakapomuona daktari,
  4. Hakikisha unamuuliza mmiliki kama mbwa huyo ana chanjo na ikiwezekana akuonyeshe kadi ya chanjo, na kama ni mbwa koko au anayejulikana kuwa na ugonjwa basi ni vyema ukawahi haraka iwezekanavyo kwenda kliniki.

Yatakayofanyika hospitalini

Daktari au manesi wauguzi watakusafisha majeraha tena na kukuchoma sindano za chanjo za kichaa cha mbwa na tetenasi. Pia wataangalia kama majeraha hayo yanafaa kushonwa hasa majeraha ya usoni au majeraha makubwa, lakini mara nyingi majeraha hayo kuachwa wazi. Pia kuna uwezekano mkubwa kuwa utaanzishiwa dama za maumivu na antibayotik.

 Dalili za kichaa cha mbwa 
  • mafua ya ghafla,
  • homa kali na maumivu ya misuli,
  • kupata ganzi sehemu ya jeraha,
  • kukosa hamu ya kula,kichefuchefu na kutapika,
  • kukosa nguvu au kuparalaizi kwa misuli hasa ya koo, taya, mfumo wa upumuaji na miguu na mikono, 
  • kuwa na dalili za pindupindu(seizure),
  • kuongea vitu visivyojulikana, 
  • kupata tabu ya kupumua.
Pindi utakapokuwa na dalili hizi daktari atalazimika kukurifaa au kukulaza kwa matibabu zaidi. 

Kama hauna dalili hizo hapo juu na haukulazwa hospitali hakikisha unatumia dawa ulizoandikiwa hadi ziishe na kusafisha vidonda mara kwa mara . Rudi tena kwa daktari baada ya kumaliza dawa ili kufanyiwa uchunguzi tena na kujua kama kuna ulazima wa kuendeleza dozi au la.

Namna ya kujikinga na Kichaa cha Mbwa
  1. Mbwa na paka ni lazima wawe wanafanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara na kuchanjwa,
  2. Ripoti mbwa ambaye anaonyesha dalili zisizo za kawaida kama kuwa mkali na kushambulia watu bila kubughudhiwa na kuwatenga mbwa na paka wote wa eneo hilo,
  3. Usimsumbue mbwa anapokula au kulisha watoto wake,
  4. Usimpige mbwa, kumvuta mkia au kumrushia mawe,
  5. Kimbilia hospitali unapong'atwa na mbwa ili kupata tiba.
Ni vigumu kufahamu kama wanyama hao wana virusi au la kwani sio kila wakati huonyesha dalili za ugonjwa huo. Usipotibiwa kwa wakati ugonjwa huu kushambulia mfumo wa fahamu na kushababisha mtindio wa akili au hata kifo. Kumbuka kinga ni bora kuliko tiba.












Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ualbino (Albinism)

 Ualbino ni nini? Ualbino ( albinism ) ni hali ya kiafya inayotokana na mwili kukosa uwezo wa kutoa homoni aina ya melanin . Homoni hii pamoja na kazi nyingine inahusika na utoaji wa rangi ya mwili. Ukosefu wa melanin huathiri ngozi, macho na nywele.  Ualbino ni hali ya kurithi kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Ikumbukwe kuwa  Albino sio mgonjwa bali ni mlemavu wa macho, nywele na ngozi ambavyo huathiri maisha yake ya kila siku, hata kufupisha umri wa kuishi. Nje na binadamu ualbino unaathiri pia wanyama, samaki, wadudu, nyoka, mijusi, ndege na hata mimea (kwa mimea hutokana na ukosefu wa klorofili).  Waathiriwa wenyewe nchini Tanzania waliamua kupendelea kuitwa "watu wenye ualbino" kutokana na matumizi mabaya ya neno zeruzeru katika utamaduni wa Afrika ya Mashariki ambako watu mara nyingi waliona uhusiano kati ya waathiriwa na mapepo au mizimu. Kuenea kwa Ualbino Tafiti zinaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya 20,000 duniani ni albino, lakini kwa sababu zisizofahamika ba...

Ugonjwa wa Fistula ( Rectovaginal Fistula)

  Fistula ni nini? Fistula ni tundu lisilo la kawaida ambalo hutokana na kuungana kwa sehemu ya chini ya utumbo mpana (njia ya haja kubwa) na njia ya mkojo au njia ya uke, hivyo kumfanya mgonjwa kushindwa kuzuia haja au kutokwa na hajak ubwa ukeni.  Mara nyingi husababishwa na kujeruhiwa kwa sehemu hizo wakati wa kujifungua hasa kwa wanawake wanaozaa katika umri mdogo au wanaokosa msaada stahiki wakati wa kuzaa. Kwa mujibu wa shirika la afya duniani,  inakadiriwa kuwa wanawake zaidi ya milioni mbili kutoka Afrika na Asia wanaishi na ugonjwa huu, bila kupatiwa matibabu yoyote, kwa upande wa Tanzania wengi wamekua wakitafuta msaada kwa waganga wa jadi.   Nini Husababisha Fistula? Ugonjwa wa Fistula unaweza kusababishwa na mambo kadhaa ikiwemo yafuatayo; Majeraha wakati wa kujifungua, Maambukizi ya Mfumo wa uzazi (PID), Mgonjwa ya utumbo mpana kama vile Crohn , Saratani ya mfumo wa uzazi au utumbo mpana, Majeraha yanayotokana na ajali au upasuaji wa sehemu ya nyonga. Fi...

Saratani ya Matiti (Breast Cancer)

Utangulizi Saratani ya Matiti ni nini? Ni aina ya saratani inayoathiri matiti au maziwa kwa mwanamke au nadra pia kwa mwanaume. Hii hutokana na chembehai( cells) za sehemu yoyote ya ziwa au yote mawili kukua kuliko kawaida na kusababisha uvimbe, maumivu, kutokwa na majimaji,damu au usaha kwenye matiti. Wakati mwingine aina hii ya saratani inaweza kusambaa sehemu nyingine za mwili kama vile kwenye kwapa, misuli ya kifua, mishipa ya damu, shingoni n.k.  Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2020, wanawake milioni 2.3 waligunduliwa kuwa na saratani ya matiti, takriban laki saba walifariki kwa saratani ya matiti. Kutoka mwaka 2015 hadi 2020 wanawake milioni 7.8 waligunduliwa kuwa na maradhi hayo, kuifanya saratani ya matiti kuwa ya kwanza kwa kuenea duniani. Ni muhimu kutambua kwamba sio kila uvimbe uliopo kwenye maziwa ni saratani, hivyo ni vyema kumuona Daktari unapokuwa na dalili yoyote nitakayotaja hapo chini kwa ajili ya uchunguzi zaidi.  Nini husababisha sarata...