Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Ualbino (Albinism)


 Ualbino ni nini?

Ualbino (albinism) ni hali ya kiafya inayotokana na mwili kukosa uwezo wa kutoa homoni aina ya melanin. Homoni hii pamoja na kazi nyingine inahusika na utoaji wa rangi ya mwili. Ukosefu wa melanin huathiri ngozi, macho na nywele. 




Ualbino ni hali ya kurithi kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Ikumbukwe kuwa  Albino sio mgonjwa bali ni mlemavu wa macho, nywele na ngozi ambavyo huathiri maisha yake ya kila siku, hata kufupisha umri wa kuishi. Nje na binadamu ualbino unaathiri pia wanyama, samaki, wadudu, nyoka, mijusi, ndege na hata mimea (kwa mimea hutokana na ukosefu wa klorofili). 






Waathiriwa wenyewe nchini Tanzania waliamua kupendelea kuitwa "watu wenye ualbino" kutokana na matumizi mabaya ya neno zeruzeru katika utamaduni wa Afrika ya Mashariki ambako watu mara nyingi waliona uhusiano kati ya waathiriwa na mapepo au mizimu.

Kuenea kwa Ualbino

Tafiti zinaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya 20,000 duniani ni albino, lakini kwa sababu zisizofahamika barani Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara kuna idadi kubwa zaidi ya albino kuliko kokote duniani. Kwa mfano inasadikiwa kwa nchini Tanzania kuna albino mmoja kwa kila watu 1,400. Nchi ya Zimbabwe inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi, ikiwa na albino mmoja kwa kila watu 1,000. 

Asili

Albino huzaliwa na hali ya kukosa uwezo wa kujenga homoni ya melanin ambayo ni muhimu kama kinga dhidi ya mionzi ya jua. Watu wenye ualbino huwa na nywele nyeupe au njano, na ngozi nyeupe. Macho yao ni bluu au hata pinki.
Uwezo wa kutengeneza homoni au pigimenti ya melanin hutegemea vinasaba (genes) vya kurithi. Vinasaba hivi vikiwa vibovu ndio husababisha mwili kushindwa kutoa melanin. 
Ikumbukwe kuwa vinasaba  hivi vibovu hubebwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Kwa kuwa vinasaba hivi vinatoka kwa baba na mama, inamaanisha kwamba mtu huzaliwa albino kama wazazi wote wawili tayari wana vinasaba vibovu. Wazazi hao wote wanaweza kuwa ni wabebaji tu na sio albino. Watoto wengine pia wanaweza kuwa sio albino. Hali hii inaendelea katika familia na inaweza kuonekana mara kwa mara inategemea na kupatikana kwa vinasaba  husika katika wazazi wote wawili.


Dalili

Ni rahisi kumtambua albino kutokana na ngozi  na nywele  zake kuwa nyeupe kuliko kawaida. 
  • Kupata majeraha kirahisi na pia kuchelewa kupona, 
  • Kupata majeraha baada ya kukaa muda mrefu juani,
  • Kuwa ma mabaka meusi ambayo hutokwa na damu kirahisi, 
  • Nywele nyeupe, nyekundu au kahawia,
  • Macho ya bluu au pinki.

Kutokana na macho kushindwa kuchuja mwanga wa jua kwa kukosekana au upungufu  wa melanin kwenye mboni, hali hii huathiri sana uwezo wake wa kuona. Vilevile hushindwa kutambua ukaribu au umbali wa kitu na kutofautisha rangi. Hii inaweza kuwa hatari hasa kwa magari na taa za barabarani.


Tiba

Kwa bahati mbaya ualbino ni hali isiyotibika. Tiba yake hulenga zaidi kwenye vitu au hatua zinazochukuliwa ili kuboresha maisha yake kama vile kuona na kinga dhidi ya jua au majeraha. 

Mambo kadha kama yafuatayo yanaweza kufanywa;
  • kufanyiwa vipimo vya macho mara kwa mara na kupatiwa miwani maalumu inayorekebisha kuona na kupunguza mwanga.
  • kufanyiwa vipimo vya ngozi kila mwaka ili kutibu majeraha pamoja na kugundua endapo kuna madoa yanayoweza kuwa na tabia ya saratani ya ngozi kutokana na mionzi mikali ya jua.



Albino anaweza kufanya yafuatayo ili kujilinda yeye mwenyewe;
  • Kuvaa miwani ya jua (sunglasses),
  • Kuvaa nguo zinazoakisi mwanga na kumlinda kutokana na mionzi,
  • Kupaka mafuta malumu yaliyotengenezwa kwa ajili ya  kupunguza athari za mionzi ya jua,
  • Kuepuka tabia hatarishi kama vile ulevi, mihadarati, ugomvi n.k,
  • Kupunguza kutoka nje wakati wa jua kali au kutumia kofia pana au mwamvuli.


Kwa wanafunzi hasa wa shule za msingi, ni muhimu walimu kuwaelimisha wanafunzi wenzake juu ya hali ya albino ili kushirikiana nae katika kuboresha maisha yake.

Hatua zingine ni kama vile;
  • kuepuka unyanyapaa,
  • kukaa dawati la mbele,


  • mwalimu kuandika kwa maandishi makubwa,
  • kutumia daftari lenye rangi iliyofubaa ili kupungua kuakisi mwanga, pia kuepuka kutumia rangi mbalimbali katika maandishi,
  • kuweka mapazia darasani na kupunguza mwanga( taa za umeme za kwenye dari),
  • kumpa muda zaidi hasa wakati wa mtihani.

Hitimisho

Kwa bahati mbaya katika jamii nyingi hasa katika bara la Afrika kumekuwa na imani duni za kishenzi zinazohusisha ualbino na mapepo, mizimu au ushirikina. Hapa kwetu Tanzania, Burundi n.k kumekuwa na imani potofu kuwa viungo vya albino vinaleta bahati kama vile mali, hivyo kusababisha mauaji ya kikatili yasiyokubalika ya albino. Ni changamoto ya kila binadamu kutoa elimu sahihi juu ya suala hili ili kulinda maisha wa wenzetu wasio na hatia. 












Maoni

  1. Asante sana kwa makala nzuri Daktari bila shaka tunaruhusiwa kushare na wengine keep it up

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ugonjwa wa Fistula ( Rectovaginal Fistula)

  Fistula ni nini? Fistula ni tundu lisilo la kawaida ambalo hutokana na kuungana kwa sehemu ya chini ya utumbo mpana (njia ya haja kubwa) na njia ya mkojo au njia ya uke, hivyo kumfanya mgonjwa kushindwa kuzuia haja au kutokwa na hajak ubwa ukeni.  Mara nyingi husababishwa na kujeruhiwa kwa sehemu hizo wakati wa kujifungua hasa kwa wanawake wanaozaa katika umri mdogo au wanaokosa msaada stahiki wakati wa kuzaa. Kwa mujibu wa shirika la afya duniani,  inakadiriwa kuwa wanawake zaidi ya milioni mbili kutoka Afrika na Asia wanaishi na ugonjwa huu, bila kupatiwa matibabu yoyote, kwa upande wa Tanzania wengi wamekua wakitafuta msaada kwa waganga wa jadi.   Nini Husababisha Fistula? Ugonjwa wa Fistula unaweza kusababishwa na mambo kadhaa ikiwemo yafuatayo; Majeraha wakati wa kujifungua, Maambukizi ya Mfumo wa uzazi (PID), Mgonjwa ya utumbo mpana kama vile Crohn , Saratani ya mfumo wa uzazi au utumbo mpana, Majeraha yanayotokana na ajali au upasuaji wa sehemu ya nyonga. Fi...

Saratani ya Matiti (Breast Cancer)

Utangulizi Saratani ya Matiti ni nini? Ni aina ya saratani inayoathiri matiti au maziwa kwa mwanamke au nadra pia kwa mwanaume. Hii hutokana na chembehai( cells) za sehemu yoyote ya ziwa au yote mawili kukua kuliko kawaida na kusababisha uvimbe, maumivu, kutokwa na majimaji,damu au usaha kwenye matiti. Wakati mwingine aina hii ya saratani inaweza kusambaa sehemu nyingine za mwili kama vile kwenye kwapa, misuli ya kifua, mishipa ya damu, shingoni n.k.  Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2020, wanawake milioni 2.3 waligunduliwa kuwa na saratani ya matiti, takriban laki saba walifariki kwa saratani ya matiti. Kutoka mwaka 2015 hadi 2020 wanawake milioni 7.8 waligunduliwa kuwa na maradhi hayo, kuifanya saratani ya matiti kuwa ya kwanza kwa kuenea duniani. Ni muhimu kutambua kwamba sio kila uvimbe uliopo kwenye maziwa ni saratani, hivyo ni vyema kumuona Daktari unapokuwa na dalili yoyote nitakayotaja hapo chini kwa ajili ya uchunguzi zaidi.  Nini husababisha sarata...