Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Vidonda vya Tumbo (Peptic Ulcers)


Ni vidonda vinavyotokea kwenye ukuta wa ndani wa tumbo au utumbo mwembamba.  Hutokana na tindikali(stomach acids) zinazotolewa na tumbo kusaidia mmeng'enyo wa chakula kuzidi hivyo kuharibu ukuta wa tumbo au utumbo mwembamba. 




Watu wengi wanaweza kuwa vidonda vya tumbo bila kuwa na dalili zozote. Lakini wakati mwingine vidonda vinaweza kutoka damu hadi kuhatarisha maisha kama hatua za dharura hazitachukuliwa.



Sababu

  • Sababu kubwa ya vidonda vya tumbo ni maambukizi ya bakteria anayefahamika kwa jina  la Helicobacter pylori(H. pylori). 
  • Matumizi ya dawa za maumivu kama vile ibuprofen(advil,ibucold, motrin IB n.k), aspirin, na naproxen  kwa muda mrefu.
  • Pombe na sigara.


Msongo wa mawazo na matumizi ya viungo vya chakula havisababishi vidonda vya tumbo lakini vinazidisha dalili za maumivu kwa mtu ambaye tayari ana vidonda.


Dalili




  • Maumivu ya tumbo sehemu iliyopo  kati ya kitovu na kifua, hasa wakati wa njaa kama vile usiku au kati ya mlo mmoja hadi mwingine. Maumivu hupungua baada ya kula au kutumia dawa za anti-asidi lakini baada ya muda huanza tena,
  • Kichefuchefu,
  • Kukosa hamu ya kula,
  • Kucheua mara kwa mara au kupatwa na kiungulia,
  • Kushindwa kula vyakula vya mafuta,
  • Kutapika damu au kupata choo chenye damu au rangi nyeusi,
  • Kujisikia unyonge au kuzimia,
  • Mwili kupungua uzito bila sababu.
Una hatari zaidi ya kupata vidonda vya tumbo kama una haya yafuatayo:
  • Una umri wa miaka 65 au zaidi,
  • Una maambukizi ya vimelea vya H. pylori,
  • Unatumia dawa za maumivu zaidi ya aina moja,
  • Ulishawahi kupata vidonda vya tumbo kabla,
  • Unatumia dawa za steroid.

Pindi utapata dalili mojawapo au kadhaa kati ya hizo hapo juu, daktari atakuuliza kama umetumia kwa muda mrefu dawa za maumivu. Majibu yako yanaweza kutosha kuanzisha matibabu ya anti-asidi na dawa za kupunguza utoaji wa tindikali (PPI). 

Daktari hulazimika kufanya vipimo vya ziada kama dalili zimezidi au mgonjwa ana hali mbaya. Vipimo hivyo ni kama vile pumzi, kupima haja kubwa kwa ajili ya vimelea vya H. pylori. Wakati mwingine kipimo cha kamera tumboni (Endoscopy) hutumika kwa ajili ya  kuchukua sampuli ili kuangalia kama kuna vimelea na kutambua pia ukubwa wa vidonda pamoja na kupambana na tatizo la kutokwa na damu.
 

Tiba

Ili kupunguza uwezekano wa kupata vidonda vya tumbo wakati unatumia dawa za maumivu;
  • Tumia dozi ndogo kabisa ili kudhibiti dalili na uache kuzitumia mara tu unapokuwa huzihitaji tena,
  • Tumia ukiwa umeshiba,
  • Usinywe pombe au kuvuta sigara wakati unatumia dawa za maumivu,
  • Tumia dawa za kupunguza tindikali kama vile Omeprazole, Pantoprazole n.k, pamoja na anti-acids,
  • Kunywa maji safi na salama,
  • Nawa mikono wakati wa kula,
  • Jifunze kupambana na msongo wa mawazo,
  • Punguza viungo vya chakula unapokuwa na maumivu ya tumbo.
Daktari atakuandikia antibiotics ili kupambana na vimelea vya H. pylori kama vitaonekana kwenye vipimo. Aina za antibiotics na dozi  zipo nje ya makala hii. 







 Ikumbukwe kuwa watu wawili kati ya watatu dunia wana maambuki ya H. pylori lakini wengi hawana vidonda vya tumbo. 




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Ualbino (Albinism)

 Ualbino ni nini? Ualbino ( albinism ) ni hali ya kiafya inayotokana na mwili kukosa uwezo wa kutoa homoni aina ya melanin . Homoni hii pamoja na kazi nyingine inahusika na utoaji wa rangi ya mwili. Ukosefu wa melanin huathiri ngozi, macho na nywele.  Ualbino ni hali ya kurithi kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Ikumbukwe kuwa  Albino sio mgonjwa bali ni mlemavu wa macho, nywele na ngozi ambavyo huathiri maisha yake ya kila siku, hata kufupisha umri wa kuishi. Nje na binadamu ualbino unaathiri pia wanyama, samaki, wadudu, nyoka, mijusi, ndege na hata mimea (kwa mimea hutokana na ukosefu wa klorofili).  Waathiriwa wenyewe nchini Tanzania waliamua kupendelea kuitwa "watu wenye ualbino" kutokana na matumizi mabaya ya neno zeruzeru katika utamaduni wa Afrika ya Mashariki ambako watu mara nyingi waliona uhusiano kati ya waathiriwa na mapepo au mizimu. Kuenea kwa Ualbino Tafiti zinaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya 20,000 duniani ni albino, lakini kwa sababu zisizofahamika ba...

Ugonjwa wa Fistula ( Rectovaginal Fistula)

  Fistula ni nini? Fistula ni tundu lisilo la kawaida ambalo hutokana na kuungana kwa sehemu ya chini ya utumbo mpana (njia ya haja kubwa) na njia ya mkojo au njia ya uke, hivyo kumfanya mgonjwa kushindwa kuzuia haja au kutokwa na hajak ubwa ukeni.  Mara nyingi husababishwa na kujeruhiwa kwa sehemu hizo wakati wa kujifungua hasa kwa wanawake wanaozaa katika umri mdogo au wanaokosa msaada stahiki wakati wa kuzaa. Kwa mujibu wa shirika la afya duniani,  inakadiriwa kuwa wanawake zaidi ya milioni mbili kutoka Afrika na Asia wanaishi na ugonjwa huu, bila kupatiwa matibabu yoyote, kwa upande wa Tanzania wengi wamekua wakitafuta msaada kwa waganga wa jadi.   Nini Husababisha Fistula? Ugonjwa wa Fistula unaweza kusababishwa na mambo kadhaa ikiwemo yafuatayo; Majeraha wakati wa kujifungua, Maambukizi ya Mfumo wa uzazi (PID), Mgonjwa ya utumbo mpana kama vile Crohn , Saratani ya mfumo wa uzazi au utumbo mpana, Majeraha yanayotokana na ajali au upasuaji wa sehemu ya nyonga. Fi...

Saratani ya Matiti (Breast Cancer)

Utangulizi Saratani ya Matiti ni nini? Ni aina ya saratani inayoathiri matiti au maziwa kwa mwanamke au nadra pia kwa mwanaume. Hii hutokana na chembehai( cells) za sehemu yoyote ya ziwa au yote mawili kukua kuliko kawaida na kusababisha uvimbe, maumivu, kutokwa na majimaji,damu au usaha kwenye matiti. Wakati mwingine aina hii ya saratani inaweza kusambaa sehemu nyingine za mwili kama vile kwenye kwapa, misuli ya kifua, mishipa ya damu, shingoni n.k.  Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2020, wanawake milioni 2.3 waligunduliwa kuwa na saratani ya matiti, takriban laki saba walifariki kwa saratani ya matiti. Kutoka mwaka 2015 hadi 2020 wanawake milioni 7.8 waligunduliwa kuwa na maradhi hayo, kuifanya saratani ya matiti kuwa ya kwanza kwa kuenea duniani. Ni muhimu kutambua kwamba sio kila uvimbe uliopo kwenye maziwa ni saratani, hivyo ni vyema kumuona Daktari unapokuwa na dalili yoyote nitakayotaja hapo chini kwa ajili ya uchunguzi zaidi.  Nini husababisha sarata...