Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Mshtuko wa Moyo (Heart Attack)

 

Utangulizi

Mshtuko wa Moyo hutokea wakati mshipa au mishipa ya damu inayoenda kwenye misuli ya moyo inapoziba na kushindwa kuipatia oksijeni misuli hiyo. Mishipa hiyo huziba kutokana na kuongezeka kwa mafuta aina ya kolesterol kwenye kuta za mishipa hiyo iitwayo coronary arteries.



Mshtuko wa moyo ni tatizo la dharura ambalo lisiposhughulikiwa kwa haraka husababisha kifo.

Dalili

  • Kupata maumivu makali ya kifua, mikono hasa wa kushoto,shingoni, mgongoni au kwenye taya ghafla na kuhisi kama kugandamizwa na kitu kizito kifuani,
  • Kuhisi kichefu chefu,maumivu ya tumbo,
  • Kutokwa na jasho la baridi,
  • Kupatwa na kizunguzungu,
  • Kuhisi uchovu wa ghafla,
  • Kushindwa kupumua.
Sio kila mtu hupatwa na dalili hizi. Wengine husikia maumivu kidogo huku wengine dalili ya kwanza ni moyo kusimama.Lakini mara nyingi mtu akipatwa na dalili kadhaa kati ya hizo hapo juu kuna uwezekano mkubwa kuwa amepatwa na mshtuko wa moyo.



Sababu

Kama nilivyosema kwenye utangulizi,mshtuko wa moyo hutokea baada ya misuli ya moyo kukosa hewa ya oksijen. Hii hutokea kwa sababu mbalimbali kama vile;

  • Mishipa kuziba kutokana na kuwa na mafuta mengi ndani yake,
  • Mishipa ya damu kusinyaa,
  • Damu kuganda ndani ya mishipa,
  • Misuli kuwa mikubwa kutokana na ugonjwa sugu wa moyo(chronic heart failure).
Watu wenye hatari ya kupata mshtuko wa moyo;

  • Watu wanene-hutokana na wao kuwa na mafuta mengi katika viungo kama vile maini,moyo,mishipa na ngozi,
  • Watu wenye kisukari- kisukari huzuia mwili kutumia mafuta hivyo kusababisha limbikizo la mafuta. Lakini pia sukari nyingi husababisha damu kuwa nzito hivyo kuhatarisha mishipa kuziba,
  • Watu wenye shinikizo la damu,
  • Uvutaji wa sigara,
  • Umri-kadri umri unavyoongezeka ndio kuna hatarishi ya kupata mshtuko wa moyo,
  • Matumizi ya madawa ya kulevya kama kokain ,
  • Historia ya familia- mshtuko wa moyo ni miongoni mwa magonjwa ya kurithi ingawa sababu zake bado hazijulikani kitaalamu,
  • Msongo wa mawazo,
  • Kukosa mazoezi.
Nini cha kufanya unapohisi dalili:
Kama mtu aliye karibu yako ana maumivu makubwa ya kifua au dalili hizo hapo juu;
  • Piga simu namba 114 (kwa Tanzania) kama hakuna uwezekano wa kuja ambulansi kama vile trafiki kubwa au vijijini mkimbize  hospitali au kituo cha afya kilicho karibu na hapo ulipo.
  • Kama inawezekana mpe kidonge kimoja cha aspirini (100 hadi 300 mg) atafune. 
  • Kama mgonjwa anajulikana kuwa na ugonjwa wa moyo na ana dawa zake anaweza kutumia kidonge cha nitroglycerine.
Dawa za maumivu kama ibuprofen au panadol hazina faida na zinaweza kuleta madhara zaidi. 

Msaada wa haraka kwa mwenye mshtuko wa moyo unahitajika ili kuokoa moyo pamoja na kuepuka kuharibika kwa misuli au mfumo wa umeme wa moyo.

Kama ilivyo kwa magonjwa mengi sugu unaweza kuepuka mshtuko wa moyo kwa kuzingatia afya yako kama vile;
  • Kufanya mazoezi 
  • Kula chakula bora na mlo kamili
  • Kupima mara kwa mara vitu kama kiasi cha mafuta(Kolesterol,Trigliserid), sukari, Pressure na mapigo ya moyo
  • Kuepuka vitu hatarishi kama uvutaji wa sigara,matumizi ya madawa ya kuvevya nk
  • Kwa wenye magonjwa sugu kama magonjwa ya moyo,kisukari,presha,figo, homa ya ini nk watumie dawa kama walivyoshauriwa na madaktari wao na pindi wanapohisi dalili mbalimbali waende kituo cha afya kilicho karibu nao.




    Maoni

    Machapisho maarufu kutoka blogu hii

    Ualbino (Albinism)

     Ualbino ni nini? Ualbino ( albinism ) ni hali ya kiafya inayotokana na mwili kukosa uwezo wa kutoa homoni aina ya melanin . Homoni hii pamoja na kazi nyingine inahusika na utoaji wa rangi ya mwili. Ukosefu wa melanin huathiri ngozi, macho na nywele.  Ualbino ni hali ya kurithi kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Ikumbukwe kuwa  Albino sio mgonjwa bali ni mlemavu wa macho, nywele na ngozi ambavyo huathiri maisha yake ya kila siku, hata kufupisha umri wa kuishi. Nje na binadamu ualbino unaathiri pia wanyama, samaki, wadudu, nyoka, mijusi, ndege na hata mimea (kwa mimea hutokana na ukosefu wa klorofili).  Waathiriwa wenyewe nchini Tanzania waliamua kupendelea kuitwa "watu wenye ualbino" kutokana na matumizi mabaya ya neno zeruzeru katika utamaduni wa Afrika ya Mashariki ambako watu mara nyingi waliona uhusiano kati ya waathiriwa na mapepo au mizimu. Kuenea kwa Ualbino Tafiti zinaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya 20,000 duniani ni albino, lakini kwa sababu zisizofahamika ba...

    Maambukizi ya Sikio la Kati (Otitis Media)

      Utangulizi Maambukizi ya Sikio la Kati(Otitis media) ni ugonjwa wa maambukizi yanayoathiri sikio la kati. Sikio la kati ni eneo lililo nyuma ya ngoma ya sikio, ambalo lina nafasi ndogo yenye hewa inayohusiana na sauti. Watoto ndiyo waathirika wakuu wa ugonjwa huu, ingawa watu wazima pia wanaweza kuugua. Maambukizi ya Sikio la Kati inaweza kusababishwa na virusi au bakteria, na mara nyingi huja baada ya kuambukizwa kwa mfumo wa hewa kama mafua au homa. Aina za Maambukizi ya Sikio la Kati Kuna aina kuu tatu za Maambukizi ya Sikio la Kati: Maambukizi ya Sikio la Kati mapya (Acute Otitis Media - AOM) : Hii ni maambukizi ya ghafla kwenye sikio la kati yanayosababisha maumivu makali na dalili kama homa. AOM ni matokeo ya virusi au bakteria, ambapo kioevu hukusanyika kwenye sikio la kati. Maambukizi ya Sikio la Kati yenye usaha (Otitis Media with Effusion - OME) : Hali hii hutokea baada ya AOM ambapo kioevu (liquid)  kinabaki kwenye sikio la kati bila dalili za maambukizi makali. I...

    Ugonjwa wa Fistula ( Rectovaginal Fistula)

      Fistula ni nini? Fistula ni tundu lisilo la kawaida linalounganisha sehemu mbili za mwili ambazo kwa kawaida hazipaswi kuungana. Kwa wanawake, hali hii mara nyingi hutokea kati ya  sehemu za siri za mwanamke  na kibofu cha mkojo au njia ya haja kubwa , hivyo kumfanya mgonjwa kushindwa kuzuia haja au kutokwa na haja k ubwa katika  njia ya uzazi .  Mara nyingi husababishwa na kujeruhiwa kwa sehemu hizo wakati wa kujifungua hasa kwa wanawake wanaozaa katika umri mdogo au wanaokosa msaada stahiki wakati wa kuzaa. Kwa mujibu wa shirika la afya duniani,  inakadiriwa kuwa wanawake zaidi ya milioni mbili kutoka Afrika na Asia wanaishi na ugonjwa huu, bila kupatiwa matibabu yoyote, kwa upande wa Tanzania wengi wamekua wakitafuta msaada kwa waganga wa jadi.   Nini Husababisha Fistula? Ugonjwa wa Fistula unaweza kusababishwa na mambo kadhaa ikiwemo yafuatayo; Majeraha wakati wa kujifungua, Maambukizi ya Mfumo wa uzazi (PID), Mgonjwa ya utumbo mpana kama vile Cr...